Katokea wapi?

Mimi naitwa Oliver John Sadiki ni mzaliwa wa Mtwara mjini Ligula B Tanzania.

Nimesoma shule ya msingi Ligula B mpaka darasa la tano.

Nikapata uhamisha kuhamia Dar es Salaam na nikaanza kusoma katika shule ya msingi Ushindi. Nikamaliza darasa la saba nikarudi tena Mtwara kwenda kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne, hapo sasa nikarudi tena Dar es Salaam kwa sababu nilikuwa napenda sana sanaa ya muziki na ngoma za asili na dansi.

Kafikafikaje katika Muziki?

Muziki nimeanza nikiwa nasoma Zanzibar chuo cha sanaa na kusoma kozi fupi. Nilipotoka Zanzibar nilijisikia kuwa mwanamuziki naelekea kwenye kukamilika kisanaa. Nikapenda kuendelea na sanaa kwa vitendo maonyesho ya jukwaani na ndio maana nikapenda kujiunga na WAMATA (Walio katika Mapambano na Ukimwi Tanzania). Hapo ndipo nilipata stadi za maisha na kujitambua pia nilipata misingi katika sanaa na kujiendeleza kupiga ngoma na gitaa na kusimama mbele za watu kutoa elimu ya ukimwi nikiwa najitolea. Pia niliwahi kushiriki kwenye mkutano wa dunia katika ukumbi wa ACC Arusha. Mpaka sasa bado ni mwanachma wa WAMATA.

Amekuwaje?

Sisi Tambala Band waliniona WAMATA wakanipenda nikajiunga. Hapo ndipo nilikuwa naimba, napiga marimba na jembe na kucheza pia.

Tulipata shoo katika tamasha la Sauti za Busara Zanzibar, Bagamoyo Arts Festival na pia tulienda China Suzhu kwenye tamasha la mashindano, tukawa washindi wa kwanza.

Baada ya kukaa miaka nane Sisi Tambala nikaamua kutoka kwa sababu nilijiona nina uwezo wa kuanzisha bendi yangu.

Sasa anajitegemea?

Nikaanzisha Nyota Kali Band ambayo mpaka sasa hivi inaendelea na kazi.

Hapo Nyota Kali Band nipo kama mkurugenzi na mwimbaji mkuu napiga marimba, besi gitaa na kucheza. Tulipata shoo Bagamoyo na pia Sauti za Busara. Bendi yangu ilifanikiwa kushinda katika mashindano ya Music Crossroads Tanzania na kuibuka bendi bora Tanzania ya muziki wa asili.

 

Tukapata nafasi ya kwenda kushindana kimataifa Zambia. Tukaibuka Washindi wa pili na mimi nikashinda mwanamuziki bora nikapewa zawadi ya safari kwenda Sweden na Croatia kubadilishana mawazo na wanamuziki zaidi ya 80 kwenye tamasha la Ethno.

Kashakuwa Teacher?

Nikaitwa Talent Search and Empowerment (TSE) kuwa mwalimu wa muziki, ngoma za asili na kucheza muziki wa kiafrika. TSE ni shirika ambayo linawaendeleza watoto wa mitaani, wenye madhingira magumu na yatima katika nyanja za sanaa ikiwemo maigizo, uchoraji, Hip Hop, ushonaji, mpira wa miguu, ngoma za asili, muziki, densi na kadhalika. Upande wangu wa muziki imefanikiwa kutengeneza albamu za watoto mbili na tumefanikiwa kupata nafasi katika TV kuonyeshwa video zetu.

Kila mwaka nafundisha madarasa yote ya Kwanza International School ili wanafunzi wote wapande jukuwaani katika sherehe ya kuitimu darasa la sita.

Hadi sasa anaendelea na mziki?

Sasa niko Ujerumani na familia yangu ndogo lakini bado naendela na mziki. Mji ambao naishi unaitwa Halle. Hapa nimekutana na marafiki na tumetengeneza bendi inayoitwa Teacher Oliver Band. Mwaka 2016 tumepata shoo na mwaka huu wa 2017 tunatarajia kupanda jukwaani tena.

Kwa taarifa zaidi kuhusu mimi na kazi zangu endelea kuangalia vipengele vingine.

 

Here in English